Alhamisi , 11th Feb , 2016

Waziri wa Mifugo, Kilimo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Nchemba amesema tayari serikali imeshaelekeza kamati za vijiji hadi mikoa yote nchini kupima maeneo na wayabainishe kwa ajili ya upimaji na umilikishwaji

Waziri wa Mifugo, Kilimo na Uvuvi Mhe.Mwigulu Nchemba amesema tayari serikali imeshaelekeza kamati za vijiji hadi mikoa yote nchini kupima maeneo na wayabainishe kwa ajili ya upimaji na umilikishwaji  kwa kushirikiana na  uongozi wa maeneo husika ili kuweka uhusiano salama na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo inaendelea kutokea nchini.

Waziri  Nchemba ameyasema hayo wakati akizungumza  na East Africa Radio na kuongeza kuwa  zaidi ya Asilimia 80 wanajishughulisha na kilimo na mifugo nchini lakini asilimia kubwa ya wananchi hao hawana hati ya umilikiwa ardhi.

Amesema serikali inaandaa dokezo la kupeleka baraza la mawaziri kwaajili ya kuangalia namna ya utengaji wa maeneo ya ufugaji na kilimo nchini na kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi inayosababisha vifo na maafa makubwa nchini.

Amewataka wananchi hasa wale jamii ya wakulima na wafugaji kuacha kuendelea kufanya vitendo vya chuki baina yao kwani kila mtanzania ana haki sawa ya kuishi.