Jumatatu , 10th Jun , 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hadi kufikia Machi 2024 miti milioni 266 imepandwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania Bara.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo

Dkt. Jafo amesema hayo wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Juni 10, 2024 ambapo amebainisha kati ya hiyo, miti milioni 211 imekukua, ambayo ni sawa na asilimia 79.3.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mhe. Aida Khenan aliyeuliza kuhusu utoaji wa taarifa ya mazoezi ya upandaji wa miti, Dkt. Jafo amesema Ilani ya Uchaguzi imeelekeza kila halmashauri nchini kupanda miti milioni 1.5 hivyo, takwimu hizo zinaonesha namna Serikali inavyoendelea na utekelezaji wake.

Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imetunga na inasimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ili kuzuia ukataji holela wa miti katika maeneo ya milimani na miinuko 

Amesema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kalenga aliyeuliza ni lini Serikali itatunga sheria kali ya kuzuia ukataji miti holela hasa kwenye maeneo yenye milima na miinuko ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Naibu Waziri Khamis ametaja Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mazingira Sura 191, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Misitu Sura 323 ambazo zina vifungu mahususi kuhusu hifadhi ya mazingira na Ulinzi wa milima, vilima na miinuko. 
 
Amesema sanjari na kutunga sheria, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha mazingira ya nchi yanalindwa na kuhifadhiwa vizuri zikiwemo kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Hatua za Haraka Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006 unaoweka lengo la kila wilaya kupanda miti milioni 1.5) kila mwaka na Mkakati wa Taifa wa Kupanda naKutunza Miti wa miaka mitano (2016/17 – 2020/2021). 

Ameongeza kuwa ili kuongeza jitihada za uhifadhi katika maeneo ya milima na miinuko, Ofisi ya Makamu wa Rais itashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mamlaka za Serikali za Mtaa na Sekta Binafsi katika kutoa elimu na kusimamia sheria zilizopo kwa sasa.