
Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Dk. Abdallah Possi amezitaka asasi na vyama vinavyojishughulisha na kutetea haki za walemavu kuacha tabia ya kutumia asasi hizo kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuongeza uelewa juu ya ualbino na kubainisha kuwa kumekuwepo na urasimu mkubwa katika asasi hizo jambo linalowanyima haki walengwa waliotajwa katika kuanzishwa kwa asasi hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk. Reginald Mengi ameitaka serikali ichunguze wanaohusika na ununuzi wa viungo vya albino na wanaotoa fedha kufadhili mauaji hayo ili kuweza kukomesha kabisa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Walemavu nchini Tanzania SHIVYAWATA Bi. Ummy Nderiananga amesema kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi albino wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa ajira pale wanapojitokeza kuomba kazi kwenye mashirika mbalimbali.
Tanzania inaazimisha kwa mara ya pili maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuongeza uelewa juu ya ualbino huku kundi hilo la watu likikabiliwa na changamoto ya saratani ya ngozi inayowapelekea watu wenye ulbino wengi kufariki kabla ya kufikia umri wa miaka 50.
