Alhamisi , 2nd Apr , 2015

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda ameagiza kila halmashauri ya mkoa huo, kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhifadhi mazingira.

Vitalu vya miti kwenye mradi wa upandaji miti.

Ametoa agizo hilo leo wakati alipokuwa kwenye maadhimisho ya siku ya upandaji miti Kitaifa, iliyofanyika Kimkoa Wilayani Longido.

Ntibenda amesema endapo kila kaya, vijiji na halmashauri watatekeleza kwa vitendo zoezi la kupanda miti na kuitunza, nchi itakuwa na hali ya hewa nzuri na mazingira yatakuwa safi, tofauti na sasa.

Aidha amesema ili kuvutia na kuhimiza zoezi hilo kwa wananchi, halmashauri inaweza kubuni njia ya utoaji zawadi kwa kila kaya itakayoongoza kupanda miti mingi na kutolewa siku ya maadhimisho hayo.

Hata hivyo amewaasa wananchi kwa sasa kulima mazao yanayokomaa kwa muda mfupi, kutokana na mvua kuchelewa kuanza.

Naye Afisa Maliasili wa Mkoa wa Arusha, Julius Achiula amesema, maadhimisho hayo yanafanyika ili kuhimiza wananchi umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni biashara ya miti panda miti uongeze kipato cha familia na hifadhi mazingira.

Chiula amesema lengo la Mkoa kupanda miti milioni 10.5 kila mwaka kupitia halmashauri zao.