Jumatano , 4th Mar , 2020

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Foka Dinya, amesema kutokana na ajali ya gari lililogongana uso kwa uso na Lori la kampuni ya Dangote na kuua watu saba,hadi sasa ni miili miwili ndiyo imeweza kutambuliwa kwa majina, kutokana na vitambulisho vilivyokutwa kwenye mifuko yao.

Mnara wa Mkoa wa Lindi

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Machi 4, 2020, Kamanda Dinya amesema kuwa vijana hao saba walikuwa wakielekea wilayani Luangwa katika biashara zao, kwani walikuwa wamefungua mradi wa kutengeneza samani za ndani.

"Chanzo cha ajali ni mwendokasi wa gari ndogo, na walikuwa ni wafanyabiashara wana mradi wao wa kutengeneza Furniture Luangwa, miili yote saba imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wawili vitambulisho vyao vilikutwa kwenye mifuko yao ya suruali ndio wameweza kufahamika, watano bado hawajafahamika" amesema Kamanda Dinya.

Ajali hiyo ilitokea jana Machi 3, 2020, majira ya 12:00 Alfajiri, katika Kijiji cha Mavuji, Wilaya ya Kilwa, ambapo gari ndogo aina ya Hiace iligongana uso kwa uso na Lori la Kampuni ya Dangote, baada ya dereva wa gari ndogo kushindwa kuimudi vizuri gari yake wakati anakwepa shimo.

Waliotambulika ni dereva Jerome Goefrey Kileo pamoja na Christopher Kitigo.