
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Nyasebwa Chimagu katika mazungumzo na East Africa Radio ambapo amesema kupitia majadiliano yatakayofanyika, kila aliye kwenye mnyororo wa thamani atapiga hatua kwa kujifunza teknolojia bora zaidi.
Aidha, amesema ili kuongeza tija katika kilimo na uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini, serikali imeitengea Wizara ya Kilimo kiasi cha TZS. Bilioni 970 ambazo zinaelekezwa kwenye maeneo mbalimbali ya kipaumbele kuhusiana kilimo cha umwagiliaji.
"Umwagiliaji ni muhimu kwa sababu wakulima wengi wanapata changamoto kwenye kuongeza tija kutokana na kutegemea zaidi mvua, katika mpango wa umwagiliaji, kuna mambo makubwa yanakwenda kufanyika kama vile kuboresha na kujenga skimu za umwagiliaji ambazo vyanzo vyake ni mito sambamba na kujenga mabwawa" amesema Nyasebwa Chimagu.
Katika hatua nyingine, Bw. Chimagu amesema kutokana na mwelekeo wa dunia kwa sasa kutumia TEHAMA, sekta ya kilimo nchini bado haijaachwa nyuma kwani matumizi ya TEHAMA yanatumia kurahisisha kazi, kuongeza ufanisi pamoja na kupunguza gharama kwenye shughuli za kilimo.
"Kwenye programu ya vijana moja ya vitu tunakaribisha ni kutambua vijana wenye ujuzi wa kurahisisha kilimo kiweze kuwa nafuu, mfano katika program ya uwezeshaji wanawake na vijana, wale ambao wana ubunifu mbalimbali wa teknolojia wakiwemo waliopata mafunzo kule Israel wamepewa fursa ya kushiriki kwenye programu na kuwaonyesha wenzao kuwa uwekezaji kwenye kilimo unawezekana na unalipa"
Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika ni mkutano maalumu ambao unawakutanisha wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kujadili fursa, changamoto, sera na mipango pamoja na TEHAMA ili kuhakikisha Afrika inakuwa uhakika wa chakula.