Jumatano , 21st Aug , 2024

Wazazi ambao watoto wao wanasoma Shule ya Sekondari Relini wameiomba Shule hiyo kuwapunguzia makali ya adhabu zinazotolewa kwa watoto wanaofanya makosa Kwani zinapelekea baadhi yao kukosa masomo.

Shule ya Sekondari Relini

Wakiongea na EATV wanasema adhabu ambazo zinatolewa zimekuwa zikiwaumiza hasa wenye kipato cha chini.
“Mimi mwanangu alichora ukuta akaambiwa alete rangi ndoo mbili pamoja na mafundi na Kama muda umepita mtoto anakuwa aingii darasani”, alisema Ally Omary, Baba wa mwanafunzi.

“Kisa kutofanya mtihani wa Jumamosi mwanangu akaambiwa Alipe Rim sasa nilikosa 1000/= ya Mtihani hiyo ya Rim naitoa wapi au wanatukomoa kula yenyewe ya shida leo mwanangu anapewa suspended huku nyumbani anakuja nyumbani huku atazidi kuwa mzembe “, alisema Juma Msumi, Baba wa mwanafunzi.

“Niliambiwa mwanangu karuka ukuta nikaambiwa nininue mfuko wa saruji, nilipochelewa kulipa mtoto akarudishwa sasa hivi tena alikuwa hajafanya mtihani nikalipishwa Rim hatujakaa vizuri nikaambia mwanao hajavaa tai tunampa suspension ya siku 21, akirudi awe amejirekebisha “, Jamila Hatibu, Mama wa mwanafunzi.

Kwa mujibu wa uongozi wa shule umesema kuwa adhabu hizo huwa zinachaguliwa na wazazi wenyewe, Mwenyekiti wa kamati ya shule ana lipi kuhusu hili?
“Wazazi na walimu tulikaa kikao tukakubaliana kuwa kuwepo na adhabu ili kupunguza utoro na nidhamu na tulikubaliana mtoto akitega siku moja ni tofali tano, asipohudhuria kwenye mtihani alete Rim moja na hii sio kuwakomoa bali ni kuongeza nidhamu kwa watoto wetu”, alisema Salim Suleiman, M/Kiti kamati ya wazazi.

Kwa upande wa uongozi wa shule umesema adhabu hizo zipo kwa ajili ya kulinda nidhamu na miundombinu na kuongeza ufanisi wa wanafunzi shuleni hapo.
"Kila shule ina misingi na taratibu zake na sheria ambazo tumewekewa na TAMISEMI, ambazo kwa shule za Sekondari huwa wazazi wanapewa na tukisema tuziappky huenda wanafunzi wengi hawatakuwepo shuleni, lakini pia shule na wazazi huwa wanakaa kwenye viako namna ya kuboresha nidhamu na taaluma na upande wa kuhribu miundombinu hata mimi nikiharibu natakiwa  nirekebishe", Rehema Akwilombe, Mku wa shule ya Sekondari Relini.