Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu Hajib Mchange imesema kuwa tuhuma zilizoelekezwa dhidi ya kiongozi wao zina lengo la kumfifisha katika jitihada zake za kuikosoa serikali hasa baada ya kuanza na muswada wa vyombo vya habari unaojadiliwa hivi sasa.
“Tumeshtushwa na tuhuma, kashfa, mbalimbali zilizotolewa jana na msemaji wa CCM, Ndugu Ole Sendeka, Chama chetu kinakaribisha uchunguzi juu ya mali na madeni ya kiongozi wetu, ndugu Zitto Kabwe” Amesema Mchange
“Tutafurahi uchunguzi huo ukihusisha akaunti zake za benki pamoja na mfumo wa maisha yake binafsi . Tunavitaka vyombo vya uchunguzi vianze kazi hiyo mara moja.Kama kuna kiongozi ambaye mali, madeni na akaunti zake viko wazi basi ni Zitto" Ameongeza Mchange.
Pamoja na hayo taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa mujibu wa katiba ya ACT Wazalendo inawataka viongozi wote wa chama kuweka hadharani tamko la mali zao pamoja na madeni.
Sambamba na hayo chama hicho kimemtaka msemaji wa CCM , ajikite katika hoja na hasa aishauri serikali yake namna itakavyosaidia wananchi katika Nyanja mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa dawa, ajira, elimu na mbinu za kukuza uchumi.








