473 waitwa kazini kati ya 19, 757 walioomba kazi

Jumatatu , 5th Jul , 2021

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Afya, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa serikali imewaita kazini watumishi wa afya 473 kati ya watumishi 19,757 walioomba nafasi za kazi kwenye kada mbalimbali za afya ndani ya Wizara hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Afya, Prof. Abel Makubi.

Akizungumza leo Julai 5, 2021, Jijini Dodoma Prof. Makubi amesema katika kuwapata waombaji wa kujaza nafasi zinazohitajika vigezo vya ziada vilitumika ambavyo waombaji wenye ulemavu walipewa kipaumbele, waliohitimu elimu mwaka 2018 na kurudi nyuma wenye ajira za mkataba wa muda na wenye umri chini ya miaka 45.

Profesa Makubi amesema kuwa nafasi hizo za ajira ni mgawanyo wa kada mbalimbali zinazotokana na watumishi kukoma utumishi wao kwa sababu mbalimbali kama vile kuacha kazi, kufariki ama kustaafu.

Amesema kuwa jumla ya maombi yaliyopokelewa kwenye mfumo yalikuwa 19,757 na kati ya hayo waombaji 4,760 hawakukamilisha ujazaji wa fomu hadi hatua ya mwisho hivyo maombi yaliyofanyiwa uchambuzi ni 14,997 na baada ya uchambuzi kufanyika jumla ya maombi 9,338 yalikidhi vigezo vya kuajiriwa kutokana na tangazo la serikali.