
Akizungumza na www.eatv.tv, Kamanda wa Polisi, ACP Blasius Chatanda amesema kwamba Marehemu aliyejulikana kwa jina la Mosses Malolela, 'Wadasani' alikutwa amejinyonga saa nane usiku wa Disemba 16 mwaka huu huku kukiwa hakuna ujumbe wowote aliouacha.
Kamanda Chatanda amesema kwamba marehemu Mosses (30), ni mkazi wa Mpwapwa mkoani Dodoma na kwamba bado haijajulikana ni jambo gani ambalo lilimpeleka mkoani Mtwara hivyo bado wanafuatilia.
Akijibu swali la kama marehemu Mosses ni mmoja kati wa wafanyabiashara wa Korosho wasio waaminifu, maarufu kama wanunuzi wa 'Kangomba', Kamanda Chatanda amesema, "Mpaka wakati huu hakuna taarifa zozote ambazo zinahusisha tukio hilo na suala la korosho. Kwa kuwa bado tunaendelea na uchunguzi tutajua sababu za kujinyonga ingawa siku hizi matukio ya kujinyonga yanasababishwa na mambo mbalimbali yakiwepo msongo wa mawazo, hali ya maisha lakini pia mapenzi nk, japo kwa marehemu Mosses bado hatujafahamu ni nini".
Mwili wa Marehemu Mosses upo katika sehemu ya kuhifadhia maiti mkoani Mtwara baada ya kutolewa juu ya mti ulipokuwa ukining'inia baada ya kujinyonga kwa kutumia waya.