Jumatatu , 10th Apr , 2023

Wavuvi katika soko la samaki msasani wamesema kuna kikundi cha watu wakika na mitumbwi mitatu wanakutana nacho baharini kikifanya shughuli za uvuvi haramu wa kutumia mabomu na baruti na kwamba tayari wamekuwa wakitoa taarifa huu ukiwa ni mwezi bila hatua zozote kuchukuliwa.

EATV imetembelea katika soko la samaki msasani kujua hali ya upatikanaji samaki ilivyo nakuzungumza na wavuvi ambao wameelezea kilio cha kukosekana kwa samaki kikielekezwa kusababishwa na wavuvi waliotajwa kutumia mabomu na baruti kisha kuuzwa samaki hao usiku eneo la mikindi,feri na kigamboni.

Wavuvi hao wamesema endapo serikali itaamua kuwadhibiti wavuvi hao wa mabomu wao wako tayari kwenda kuwaoneshaa eneo wanalovua samaki hao.

Hata hivyo uongozi wa soko hilo umekiri kuzipata taarifa hizo kutoka kwa wavuvi wanaoingia baharini na kuomba serikali kuchukua hatua zaidi kwa kuwa wao wanalipa leseni na tozo zote stahiki hivyo uwepo wa wavuvi haramu ni hatari kwa soko la samaki.

Baadhi ya wavuvi wamemlilia waziri husika wa uvuvi na mifugo wakimuomba kufanya doria maalum kwa kuwa kurejea kwa uvuvi wa mabomu kunafifisha jitihada za serikali kuinua uchumi wa Bluu.