Jumatatu , 5th Jun , 2023

Jaji msitaafu na Kamishina wa viapo Thomas Mihayo amewataka watendaji wenye taaluma ya sheria walioko kwenye sekta ya umma kutuliza akili katika kufanya maamuzi na ushauri kwa viongozi wakuu hasa katika masuala ya kimikataba hususani katika kipindi hiki ambacho Taifa linaita wawekezaji.

Jaji msitaafu na Kamishina wa viapo Thomas Mihayo

Mstaafu Jaji Thomas Mihayo ametoa rai hiyo kufuatia mwendelezo wa ufatiliaji wa sakata hili linaloonesha kufatiliwa zaidi na wawekezaji ambapo akipitia hukumu ya kesi iliyohusu kampuni kutoruhusu muunganiko wa kampuni mbili katika uwekezaji wa saruji kati ya kampuni ya Tanga cement na Scancerm ambao hadi sasa umeonesha kuvunjwa kwa utawala wa sheria.

Amesema zipo dalili za wazi kwamba wanasheria wa wizara walitoa taarifa zisizo sawa kwa waziri wa Uwekezaji viwanda na Biashara hali iliyopelekea kuzua utata wa kisheria usio zingatia amri ya mahakama.

Aidha Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesisitiza kuwa kwa sasa kutofuata amri za mahakama kwenye masuala ya kibiashara kunaweza kuligharimu Taifa kufuatia baadhi ya watendaji wake kuuza miiko.

Utakumbuka hivi karibuni Kampuni ya saruji ya Chalinze Cement, ilifungua kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, ili kumtaka Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), kuirudisha mara moja kampuni hiyo katika daftari la kampuni zilizosajiliwa na kutambulika kisheria nchini.

Kesi hiyo namba 113, ya Mwaka 2023 imefunguliwa na Chalinze Cement kupitia kwa Mkurungenzi Mkuu wake Mohamed Hussein Bahdera.

Itakumbukwa, baada ya vuguvugu la mida mrefu kuhusu madai ya BRELA kuifuta kampuni hiyo, hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara ilithibitisha kufutwa kwa Kampuni ya Chalinze Cement, kwa madai kuwa nyaraka zake zimegundulika kuwa za uongo wakati wa usajili na Wanahisa wa kampuni hiyo hawatambuliki.

Taarifa hiyo ilitolewa, Machi mwaka huu na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji, Bungeni Jijini Dodoma, alipokuwa akijibu hoja za wabunge wakati akihitimisha mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Hata hivyo, katika mkutano wa wanahabari uliofanyika jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita, Wakili Melchisedeki Lutema, amesema sakata hilo lilianza mara tu baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kibiashara ya Septemba 23, 2022 juu ya kuungana au kutokuungana kwa makampuni ya saruji ya Twiga na Tanga, yalieleza wazi kuwa yamezuia kuungana kwa makampuni hayo na hayakutoa muda maalumu wa kuisha kwa uamuzi huo.

Aliongeza kuwa, katika mazingira hayo Chalinze Cement walijitokeza kupinga muunganiko huo ili kulinda maslahi ya walaji na mazingira ya usawa wa soko.
Akizungumzia kufutwa kwa kampuni ya Chalinze Sementi, wakili huyo alieleza kuwa wameshangazwa na utaratibu uliotumika kwa kuwa wateja wake hawakupewa taarifa na sababu za kufutwa kwake.