Jumanne , 20th Sep , 2022

Serikali Mkoani Shinyanga imetoa onyo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa zilizomaliza muda wa matumizi kwa kubandika stika na lebo za bandia, jambo linalohatarisha afya za watumiaji wa bidhaa hizo.

Bidhaa zilizobandikwa lebo bandia

Katika taarifa hiyo, imeonekana kwamba wapo wanaotumia  vipimo vya magonjwa  visivyo na kiwango ambavyo vinatoa majibu yanayotofautiana na kulitaka shirika la viwango Tanzania (TBS) kuchukuwa hatua kali kwa watakaobainika kutumia vipimo visivyo sahihi.

Akizungumza kwenye semina ya ufahamu juu ya elimu ya metrolojia, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, amesema bado kuna changamoto kubwa kwenye vipimo vinavyotolewa kwenye maabara, pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kubandika lebo kwenye bidhaa zilizomaliza muda wa matumizi na kuziweka sokoni.

Kwaupande wake Afisa mwandamizi wa shirika la viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Johanes Maganga amesema vipimo ambavyo siyo sahihi vinaweza kusababisha madhara kwa jamii, huku Meneja wa Metrolojia Stella Mrosso akibainisha kuwa lengo la kutoa elimu kwa jamii na wadau wa biashara ni kuhakikisha jamii inakuwa salama, huku baadhi ya washiriki wa semina hiyo kutoka maabara za viwanda, hospitali na Mamlaka za maji wakisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutoa huduma bora kwa kutumia vipimo sahihi.