Jumatatu , 26th Sep , 2022

Wafanyabiashara katika soko kubwa la tikitimaji la Tazara Vetenari wamesema kuwa matunda hayo kwa sasa yanapatikana kwa wingi lakini changamoto imekuwa ni soko la uhakika na kuiomba mamlaka kuwatafutia soko nje ya nchi.

Soko la tikitimaji Tazara - Vetenari

Hatua hiyo imekuja baada ya EATV kubaini uwepo na mlundikano mkubwa wa tikitimaji sokoni hapo hupu magari yanayopakia mzigo wa matunda hayo kutoka sokoni hapo yakiwa ni kidogo kuliko mzigo uliopo hali inayoashiria kuwa manunuzi ni kidogo.

“Hivi sasa tikiti inapatikana kwa wingi sana, hapa sokoni tunasema ndilo soko kubwa zaidi Afrika Mashariki lakini changamoto ni soko la uhakika, ndani wateja siyo wengi sana, hata sasa tunaona tumepata soko Zanzibar lakini bado halitoshi kama unavyoona yamejaa hapa na hakuna wateja"- Jafari Ngoroge,  M/kiti wauza Tikiti Tazara.

 Aidha, EATV imepata fursa ya kuzungumza na Bi. Fatuma Kisanji ambaye ni mkulima wa tikitimaji kutoka Tabora ambaye amesema kwamba kilio kikubwa kwa wakulima wa tunda hilo ni gharama kubwa za usafiri.

“Wakulima wa mikoani tunapata changamoto ya usafiri, usafiri kutoka mikoani kuleta mzingo sokoni Dar es Salaam imekuwa ghari mno. Mimi kutoa gari moja la tikitimaji kutoka Tabora hadi Dar es Salaam nimelipa Milioni mbili, fikiria hiyo gharama... nitapata faida kweli?" - Alisema mkulima huyo.