Alhamisi , 16th Feb , 2023

Wafanyabiashara wa jumla wa Nafaka hususani Mchele katika soko la Tandale Dar es salaam wamesema hatua ya serikali kutangaza kuagiza Mchele nje ya nchi ni nzuri lakini wameomba uletwe sampo kidogo wajiridhishe nayo sokoni kabla ya kuagiza tani nyingi zikaozea ndani.

Siku chache tuu serikali imetoa mwongozo wa kuagiza mchele wa kutoka nje ili kuleta suluhu kwa ongezeko kubwa katika bei ya mchele ambayo kwa sasa imepanda hadi kufikia 3200 kwa kilo kwa mchele supa.

Hali hii imenifanya kukita kambi katika soko la Tandale ambalo ni maarufu kwa uuzaji wa mchele kuzungumza na wafanyabiashara ambao wamesema ubora wa mchele unaolimwa hapa huuzwa kwa msimu husika hali ambayo huuufanya ubora wake kuwa juu wenye ladha.

“Nia ya serikali kwenye kuagiza mchele kutoka nje ni nzuri shida na wasiwasi yetu ni kwa hao watakaopewa tenda ya kuagiza wasije kuleta mchele ambao huko unakotoka uwe umekataliwa ndio wanatuletea”Amesema Shabani Guni-Mfanyabiashara wa mchele wa jumla.

Kadhalika na hilo wafanya biashara hao wamesema huko nyuma tayari serikali iliwahi kuingiza michele wakitaja aine kama VIP na KITUMBO ambayo kila moja ilikuwa na changamoto zake hivyo kuomba iletwe sampo wajiridhishe.

“Unakumbuka huko nyuma serikali tayari imewahi kuagiza aina kadhaa za mchele tuliona madhara yake tumejifunza uhaba wa mchele tunao lakini tuwe makini sana kwenye hili” amesema  Salum Mfanyabiashara wa Nafaka.-Mfanyabiashara wa Nafaka.

Kwa upande wa watumiaji wa bidhaa hiyo wamesema serikali itazame ubora kwa kuwa hili ni suala la afya za watu moja kwa moja

“Niiombe serikali yangu kujikita zaidi kwenye ubora maana mfanyabiashara ni mtu anaetazama faida yake kwanza hivyo kwenye hili ubora uzingatiwe kupita kiasi”Amesema Said -Katibu wa soko Tandale.

Serikali imeombwa kufanya tathimini za mara kwa mara kupitia bodi zake za mazao mbalimbali yakiwemo nafaka ili kuwa na majibu ya mapema kuwa uhaba wa chakula uliopo unadhibitiwa mapema na sio kungojea taharuki za kupanda bei za vyakula hususani kwenye nafaka huku wakiacha swali kwamba mchele unaingia utaitwa jina gani?ukiacha VIP na KITUMBO uliowahi kuingizwa nchini.