
Dawa asilia zikiuzwa mtaani, Dar es Salaam
Wakati takwimu kutoka Wizara ya Afya zikionesha kuwa zaidi ya 60% ya Watanzania wanatumia dawa asili, hali ya upatikanaji wa dawa hizo umekuwa haupo kwenye utaratibu mzuri, hali inayowalazimu wadau wa dawa hizo kuiomba serikali idhibiti uuzaji wake.
“Ni kweli kabisa kwamba watanzania wengi tunategemea dawa asilia kutibu maradhi tuliyonayo, lakini namna dawa hizi zinavyohifadhiwa na kuuzwa imekuwa siyo nzuri na rafiki kwa afya za walaji, mfano ukipita hapa Jijini utaona watu wanziuza tu kwa kutembeza, zipo wazi bila kufunikwa, barabarani zinauzwa tu mavumbi na uchafu wa kila aina unazifikia. Niombe serikali izingatie na kusimamia sheria na taratibu za dawa hizi hawa watu waondolewe barabarani"- MWADAWA KIWASILA – Mtaalam wa dawa asilia.
Kutokana na hali hiyo, EATV imemtafuta Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Bw. Boniventura Mwalongo ambaye ambaye amesema kuwa wanafanya kazi kubwa kuwaelimisha wadau wote wa dawa hizo, na kwamba zimekuwa mhimu hasa katika kipindi cha COVID 19.
Aidha, kutokana na kuripotiwa kwa magonjwa ya mlipuko katika mataifa jirani, Bw. Mwalongo anatoa maelekezo kwa wataalam wa tiba na dawa asilia kuzingatia usafi na kanuni za afya ili kuwalinda wateja wao.