Jumatatu , 19th Aug , 2024

Wizara ya Madini imeendelea kuziaminisha sekta za fedha kuwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini nchini wanayo fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuendesha shughuli zao katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde

Hayo yamebainishwa leo Agosti 19, 2024 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde mkoani Shinyanga  katika hafla fupi ya utoaji wa mfano wa hundi ya shilingi bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa Madini ikiwa ni mkopo kutoka benki.

Waziri Mavunde amesema kuwa mikopo iliyotolewa itasaidia kuikuza na kuiendeleza Sekta  ya Madini na hivyo kupelekea kuongeza kwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye pato la Taifa na uchumi wa nchi.

Waziri Mavunde  ameipongeza Benki hiyo kwa kutoa mkopo wa Bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo na watoa huduma na kutumia fursa hiyo kuzitaka benki nyingine pia kuiunga mkono sekta ya madini kupitia utoaji wa mikopo.

Akitoa salamu, Rais Wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA) Ndg. John Wambura Bina amempongeza Rais Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya madini ambao umeanza kuleta tija na kuaminika kwa wachimbaji wadogo kukopesheka kwakuwa sasa kuna mashine za uchorongaji zinazosaidia kupata taarifa za awali za uwepo wa madini na hivyo kuwatoa wachumbaji kwenye kuchimba kwa kubahatisha.