
Kamati hiyo imefanya ziara katika Kituo cha Kinyerezi II kujionea uendeshaji wake, kabla ya kutembelea kituo hicho, kamati ilitembelea mitambo ya uzalishaji wa gesi mkoani Mtwara.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 13, 2022 baada ya kukagua shughuli zinazofanyika, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula amesema wameona jinsi kituo hicho kinavyoweza kuzalisha megawati 240 na upatikanaji wake ni stahimilivu.
"Tanesco wametuhakikishia wana mipango madhubuti ya kuhakikisha wana uwezo wa kupata vifaa kipindi chote cha mwaka bila kuwa na matatizo yoyote," amesema Kitandula.
Mwenyekiti huyo amesema wamefurahi kuona kituo hicho kinaendeshwa na Watanzania wenyewe, jambo ambalo amesema ni zuri kwa mustakabali wa taifa hili.