Jumatatu , 7th Jun , 2021

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amesema suluhu ya kudumu ya miwa ya wakulima wa Kilombero ni upanuzi wa kiwanda cha Kiwanda cha Sukari cha Ilovo, ambacho kitawasaidia kuuza zaidi miwa yao.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo,

Prof. Mkumbo amebainisha hayo katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni, leo Juni 07 ambapo amesema upanuzi huo utaongeza uzalishaji wa sukari katika Kiwanda hicho kutoka tani 127,000 kwa mwaka hadi tani 271,000 kwa mwaka ikiwa ni ongezeko la tani 144,000.

“Suluhu ya kudumu ya miwa ya wakulima wa miwa kilombero ni upanuzi wa kiwanda hiki kwani wakulima watauza zaidi miwa yao kwa sababu kiwanda kitakuwa na uwezo wakuchukua zaidi ya mara tatu ya miwa wanaochukua sasa hivi,” amesema Prof. Mkumbo.

Aidha, Prof. Mkumbo ameahidi kufuatilia uhujumu wa wakulima wa miwa uliobainishwa na Mbunge wa Jimbo la Mikumi Dennis Londo akiitaka kujua tamko la serikali juu ya wanaotaka (kiwanda) kuhujumu wakulima wa miwa na Watanzania wanaoshirikiana na wawekezaji katika hilo.

“Tamko la serikali kuhusu wawekezaji wa viwanda Serikali inataka wawekezaji wote nchini kufanya shughuli zao kwa kuzingaia sheria na kama kuna hujuma kama alivyoeleza Mheshimiwa mbunge tutafuatilia,“ amesema Waziri Kitila Mkumbo.