Ijumaa , 7th Oct , 2022

Wakati ulimwengu ukiadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, wafanyabiashara nchini wamepongezwa kwa uzalendo wao wa kujenga nchi na kuchochea maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa Watanzania.

Bwana Alphayo Kidata, Kamishna Mkuu TRA

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya mapato nchini Tanzania Bwana Alphayo Kidata akiwa anasherekea huduma kwa wateja Jijini Dar es Salaam, amesema kinachofanywa na wafanyabiashara nchini ni uzalendo wa hali ya juu kwakuwa makusanyo ya kodi ndiyo yanatumika kuijenga nchi.

“Ili nchi ipate maendeleo ni lazima tukusanye kodi, kodi hii ndiyo inayojenga miundombinu na miradi mingine. Kwahiyo wafanyabiashara nchini wamekuwa wanaonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kuwasilisha kodi ambazo ndizo chanzo cha maendeleo yote haya. Mfano katika mwaka huu tumepangiwa kukusanya Trilioni 23 na kwa robo hii tulipanga kukusanya Trilioni 5 na tumekusanya kwa 99.1%.” - Bwana Alphayo Kidata, Kamishna Mkuu TRA.

Aidha, mmoja wa Wafanyabiashara Katika Jiji la Dar es Salaam ameiomba mamlaka ya mapato kupunguza masharti ya utoaji mashine kwa wateja kama ilivyo hivi sasa.

“Kwanza nimpongeze Kamshna kwa kututembelea, mimi kama Mfanyabiashara nimuombe sasa mamlaka ipunguze masharti na taratibu za utoaji mashine kwa wafanyabiashara, tunatumia muda mrefu sana kupata mashine, hii si sawa. Niombe walifanyie kazi kama kweli wanataka kila Mfanyabiashara awe na mashine"- Bukuye Bukuye,  Mfanyabiashara Dar es Salaam.