Alhamisi , 21st Jul , 2022

Serikali imepanga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini kwa kuvutia wawekezaji wengi duniani kuja kuwekeza katika sekta  hiyo na kufungua fursa nyingi za kuchimba madini

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko alipokutana na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika mkutano uliolenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za uchimbaji  Julai 20, 2022 mkoani Kigoma.

Dkt. Biteko amesema, mataifa mengi yanakuja nchini kujifunza kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini na hasa sekta ndogo ya wachimbaji wadogo na hivyo kuifanya Tanzania kuwa mfano kwa mataifa.

Amesema Serikali imeendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji katika Sekta ya Madini kuweza kuwekeza katika uchimbaji wa madini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara hiyo.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wachimbaji wadogo wapo kwenye moyo wake, tena anawaita wachimbaji wangu wadogo, anawapenda na kuwathamini sana, anatamani kuona changamoto walizonazo wachimbaji hao kote nchini zinamalizwa kwa haraka," amesema.

Akizungumzia mikopo kwa wachimbaji wa madini, Dkt. Biteko amesema Serikali imefanya kazi kubwa kuzungumza na taasisi za fedha ili zianze kukopesha wachimbaji wadogo na tayari zipo baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo kwa wachimbaji.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa, Sekta ya Madini ina wajibu wa kutoa ajira kwa Watanzania, kukuza uchumi wa nchi na kujenga utajiri na kuwaondolea umaskini watu.

Amesema, changamoto ya soko kuu la madini la mkoa linaloendelea kujengwa Serikali itakamilisha ujenzi wa soko ili watu wengi waweze kuleta madini yao kuuza madini yao hususan wafanyabiashara kutoka nchi za jirani.

"Serikali itaendelea kufanya utafiti kwenye maeneo yanapochimbwa madini nchini ili wachimbe na kupata manufaa,"ameongeza. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe.Thobias Andengenye amewapongeza wachimbaji wa mkoa wa huo kwa kufanya kazi na kuendelea kuutangaza mkoa kwa uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Kigoma (KIGOREMA) Lister Balegele amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa na viwango vya kutoa tija katika soko la ndani na nje ya nchi na kudhibiti uchimbaji holela wa madini usiofutata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Serikali.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Kigoma Mhandisi Pius Lobe amesema, mkoa wa Kigoma una jumla ya leseni 429 za uchimbaji mdogo wa madini, leseni mbili za uchimbaji wa kati wa madini. Nyingine ni leseni tisa za utafutati mkubwa wa madini, leseni nane za biashara ndogo ya madini na leseni 11za biashara kubwa ya madini.

Mkoa wa Kigoma una aina mbalimbali za madini katika maeneo mbalimbali ikiwemo madini ya ujenzi, madini ya metali,viwandani na ya vito.