Jumatatu , 10th Sep , 2018

Imeelezwa kuwa tofauti ya bei za mafuta kati ya Dar es salaam na Tanga ni kutokana na mkoa huo kuwa na mafuta ambayo yalinunuliwa kwa bei kubwa mwezi Mei ambayo mpaka sasa shehena yake haijaisha na si kwamba bei zimepanda kama inavyodaiwa.

Pichani gari likijazwa mafuta.

Akizungumza kwenye East Africa BreakFast ya East Africa Radio, afisa habari wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguwo amesema kuwa bandari inayolisha mikoa ya Kaskazini bado haijamaliza mafuta yaliyochukuliwa kwa gharama kubwa na itapungua wakimaliza na kuagiza mapya.

Sasa hivi tunatumia bandari tatu, zikiwemo bandari ya Dar es salaam, Mtwara na Tanga na matumizi ya kila bandari yanatofautiana kutokana na idadi ya watu na matumizi yake, Dar es salaam inahudumia sehemu kubwa ya nchi hivyo mzigo ulioingia kwa gharama kubwa umeshakwisha lakini Tanga bado wana mzigo uliopita wala bei haijapanda”, amesema Kaguwo.

Septemba 5, 2018 Ewura ilitangaza kushuka kwa bei za rejareja za Petroli, Dizeli na mafuta ya Taa kwa asilimia 0.43 (shilingi 10) na asilimia 0.83 (shilingi 19) na asilimia 1.05 (shilingi 24 kwa lita) huku bei za rejareja za Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini zimeongezeka kwa shilingi 114/lita (sawa na asilimia 5.11) na shilingi 102/lita (sawa na asilimia 4.70).