Jumamosi , 22nd Oct , 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi kama kichocheo cha kukuza sekta ya utalii hapa nchini hivyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuleta mageuzi hususani katika sheria na maboresho ya sera ya bajeti.

Makamu wa Rais Tanzania Dkt. Philip Mpango

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 22 Oktoba 2022 wakati wa ufunguzi wa onesho la sita la kimataifa la utalii la Swahili (Swahili International Tourism Expo) linalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mlimani city jijini Dar es salaam.

Dkt. Mpango ametaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ikiwemo kuboresha miundombinu ya huduma za utalii ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi, kujenga na kukarabati barabara, viwanja vya ndege, kambi za watalii na kuongeza kasi ya shirika la ndege la Taifa ili kurahisisha safari za ndani ya Tanzania pia.

Aidha amesema Utalii ni miongoni mwa sekta zinazopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa bingwa wakuimarisha sekta hiyo baada ya Uviko-19, kupitia makala ya ubunifu ya The Royal Tour ambayo imepelekea matokeo chanya ya kuongezeka kwa watalii na mapato nchini.