Jumanne , 18th Oct , 2022

Nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC+ zimekubaliana kwa pamoja kuidhinisha hatua ya kupunguza kiwango cha uzalishaji mafuta, licha ya Marekani kuikemea hatua hiyo na kusema imechochewa kisiasa.

Hatua hiyo ya nchi wanachama wa OPEC+ imeidhinishwa rasmi jana licha ya onyo la Marekani. Washington imekuwa ikiishutumu Saudi Arabia kula njama na Urusi na kuyashinikiza mataifa mengine kuunga mkono hatua hiyo ambayo inasema itaongeza mapato ya kigeni ya Urusi na kupunguza makali ya vikwazo vya mataifa wa Magharibi dhidi ya Urusi.

Saudia hata hivyo imekanusha leo kuiunga mkono Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine, huku Waziri wa nishati wa jimbo la Ghuba Suhail al-Mazrouei akisema kuwa uamuzi wa OPEC+ ambao uliidhinishwa kwa kauli moja, ulikuwa wa kiufundi na usiyo na malengo yoyote ya kisiasa.

Mfalme wa Saudia Salman bin Abdulaziz amesema Ufalme huo unawajibika kwa bidii ili kusaidia utulivu na usawa katika masoko ya mafuta, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kudumisha makubaliano ya muungano wa nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC+.