Jumatatu , 12th Jun , 2023

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekutana na ujumbe kutoka Misri, ambao umesema kwamba umepanga kuanzisha machinjio ya kisasa hapa nchini yatakayowezesha kusafirisha tani 600 za nyama pamoja na wanyama hai wakiwemo ng'ombe, kondoo na mbuzi 10,000 kila mwezi.

Akizungumza hii leo Juni 12, 2023, na ujumbe kutoka nchini Misri uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Taifa ya Huduma za Miradi (NSPO) Meja Jenerali, Hossam Nigeda Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega amewahakikishia kwamba Tanzania ipo tayari na watawapa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha biashara hiyo iweze kuanza haraka iwezekanavyo.

Katika mazungumzo yao, Meja Jenerali, Nigeda ameeeleza kwamba lengo lao ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili kwa kufungua soko la nyama ya Tanzania nchini Misri na kwamba siku za hivi karibuni wapo katika mipango ya kusafirisha tani 100 za nyama kabla ya sikukuu ya Eid Al Hajj ili kuanza kutangaza soko la nyama ya Tanzania nchini humo.

Misri ni miongoni mwa nchi zenye Idadi kubwa ya watu barani Afrika ambapo Idadi ya watu wake hawapungui Milioni 120 hivyo itakuwa fursa nzuri ya kibiashara kwa Tanzania hususan biashara ya nyama.

Ziara hiyo ni miongoni mwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua milango ya kibiashara nje ya nchi.