Jumatatu , 1st Mei , 2023

Waziri wa Madini Doto Biteko, amesema moja ya vipaumbele vya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni uanzishwaji wa minada na maonesho ya madini ya vito nchini.

Madini

Hayo ameyabainisha alipokutana na kuzungumza na watumishi wa Tume ya Madini kutoka mikoa ya kimadini Morogoro na Mahenge katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei 1, 2023 mkoani Morogoro.

"Ofisi ya Madini Mahenge mnatakiwa kusimamia vizuri uchimbaji wa madini ya vito wakati wizara ikiwa mbioni kuanzisha minada na maonesho ya madini ya vito hapa nchini," ameeleza Dkt. Biteko.

Pia, amewataka kusimamia vizuri uchimbaji mkubwa wa madini ya Kinywe unaotarajiwa kuanza hivi karibuni katika maeneo hayo.

Dkt. Biteko amewataka watumishi wa wizara na taasisi zake kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya wizara, amesema watumishi hao ni taa ya wizara kuhakikisha sekta inakua na kufungamanisha sekta nyingine.