Jumanne , 22nd Nov , 2022

Tani 210 za mbegu za pamba katika kiwanda cha Jielong kinachomilikiwa na raia wa china mjini Shinyanga kimenusurika kuteketea kwa moto baada ya ghala la kuhifadhia mbegu kuanza kuwaka moto upande wa mashudu na kuunguza sehemu kubwa ya ghala hilo

Katika tukio hilo wafanyakazi wanne waliokuwa wakifanya kazi ndani ya ghala hilo wamejeruhiwa na moto na kukimbizwa hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu

Msemaji wa kiwanda cha Jielong Qir Fengzhou amesema moto huo ulianza kuwaka kidogo majira ya saa 11 jioni jana na wakaanza kuuzima lakini ghafula ulilipuka na kuwa mkubwa na kuomba msaada Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Shinyanga ambao walifika mapema kwa kushirikiana na magari mengine ya makampuni na kuanza kuzima moto huo kabla ya kusababisha madhara makubwa upande wa mbegu.

Mrakibu wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Shinyanga  Ramadhan Kano akiwa eneo la tukio,amesema wamefanya jitihada kubwa kuzima moto huo kutokana na kuwa mkubwa na kufanikiwa kuudhibiti kabla ya kusababisha madhara makubwa upande wa mbegu.