Jumatatu , 14th Nov , 2022

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amebainisha kuwa, biashara ya Makaa ya Mawe inatarajia kuleta tija kwa Watanzania kutokana na uhitaji mkubwa wa madini hayo ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa

Dkt. Kiruswa ameeleza hayo wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma alipotembelea mgodi wa uchimbaji wa Makaa ya Mawe wa Ruvuma Coal Ltd ili kujionea shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika mkoa huo.

Ameeleza kuwa, serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta ya madini yanayovutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani kuja kuwekeza na kufanya biashara ya madini mbalimbali yakiwemo Makaa ya Mawe.

Aidha ameongeza, serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa Makaa ya Mawe kutoka kwenye migodi hususani barabara ya kuelekea mkoani Mtwara ili kusafirisha Makaa ya Mawe hayo katika bandari.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo amesema, kutokana na uwepo wa migodi imesaidia wilaya hiyo kupata faida nyingi katika kutekeleza shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya.