Fedha
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, mikoa na Halmashauri, Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani alisema kuwa, Benki Kuu chini ya Wizara ya Fedha na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mikakati kupitia sheria ya huduma ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, ili kukomesha udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha kupitia mitandao ya simu.
Mnyamani alisema mikopo inayotolewa kwa njia ya mitandao ya simu imekuwa changamoto kubwa hasa katika ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji jambo linalopelekea watoa huduma hao kuvunja sheria ya usiri inayotakiwa katika kupata huduma ya fedha kwa kuwadhalilisha wakopaji hao kwa kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu na jamaa waliochukua mikopo hiyo.