Jumatano , 1st Aug , 2018

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, Prof. Mussa Juma Assad amesema kuwa atahakikisha fedha zote zinatumika ipasavyo na hatoruhusu pesa yoyote kutoka hazina bila ruhusa ya Bunge.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, Prof. Mussa Juma Assad.

Prof. Assad amesema hayo wakati akizungumzia mafanikio ambayo Tanzania imeyapata kutokana na kuwa moja ya nchi zilizofanya ukaguzi wa Umoja wa Mataifa, jukumu ambalo hivi sasa limebebwa na nchi ya Chile.

Prof. Assad amesema wakaguzi zaidi ya 200 waliohusika katika ukaguzi huo, wamejifunza mbinu za kisasa za ukaguzi, ukiwemo kujengewa uwezo kufanya ukaguzi wa mifumo ya malipo ya kielektroniki na kimtandao bila kuisababishia serikali hasara.

Ukaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa sio tu umeipatia sifa Tanzania, bali umetujengea uwezo wakaguzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, kufanya udhibiti ambapo kuanzisa sasa tutakuwa tukitoa ripoti ya udhibiti wa fedha zote katika mfuko mkuu wa hazina, ambazo zimetumika bila kuidhinishwa na Bunge”, amesema CAG.

Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2016/17 aliyoiwasilisha mwezi Machi, 2018 imeibua ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika baadhi ya taasisi za Serikali na kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi.

Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam ambayo ilizitaja taasisi zilizobainika kuwa na ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha kuwa ni, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).