Ijumaa , 15th Jul , 2016

Kasi ya vijana kuhama kutoka maeneo ya vijijini kwenda mijini nchini imeanza kupungua kufuatia mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na Chemba ya Wanawake Wajasiriamali TWCC juu ya mbinu za namna ya ufanyaji biashara.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wajasiriamali Wanawake nchini TWCC, Bi. Jaqueline Mneney Maleko akionyesha Tuzo waliyoipata katika siku ya ufunguzi wa Maonyesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Mafunzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiwalenga wanawake hususani wale wanaofanya biashara na umiliki wa viwanda vidogo vidogo, yamekuwa msaada kwa wanawake wengi ambao awali walikuwa wakikimbilia mijini kwenda kutafuta maisha bora lakini sasa wameanzisha biashara zao ambazo huzifanyia hukohuko katika maeneo wanakoishi.

Mkurugenzi wa TWCC Bi. Flora Rimoy amesema hayo jijini Dar es Salaam, katika mahojiano na EATV kuhusiana na jinsi chemba hiyo ilivyofanikiwa kuibuka mshindi wa kwanza katika kigezo cha taasisi na makampuni yaliyosaidia kujenga uwezo wa ufanyaji wa biashara au kwa kifupi Business Facilitation Award.

TWCC ni moja ya taasisi zilizoshiriki Maonyesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam na kushirikisha wafanyabiashara na makampuni kutoka ndani na nje ya nchi.

TWCC imetunikuwa tuzo ya taasisi bora inazowezesha ukuaji wa biashara katika kinyan’ganyiro cha saba kati ya vinyanganyiro zaidi ya 18 vilivyokuwa vikigombaniwa katika maonyesho hayo yaliyozinduliwa na Rais wa Rwanda Mh. Paul Kagame.

Kwa mujibu wa Bi. Flora, mafunzo wanayoyatoa yamesaidia kuwainua akina mama pamoja na wasichana wengi kutoka maeneo ya vijijini, ambao hivi sasa wanatumia fursa ya rasilimali zinazowazungukuka katika kuanzisha biashara ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua ubora wa maisha yao.

Amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni uwepo wa kiasi kikubwa cha mazao, bidhaa za kilimo na misitu, ambazo kwa kupitia mafunzo yanayotolewa na TWCC, wanawake hao wamefanikiwa kuanzisha biashara na viwanda vidogo vidogo ambavyo vimekuwa vikiongeza thamani ya mazao hayo na hivyo kuchangia juhudi za serikali za ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Aidha, wanawake wengine wamekuwa wakijishughuliza na uchimbaji na uongezaji thamani bidhaa za madini na vito, pamoja na ushonaji ambapo sasahivi wana uwezo wa kuuza bidhaa zao katika masoko ya nchi za jirani kupitia vikundi vilivyoanzishwa vya wafanyabiashara wanawake katika maeneo yote ya mipakani.

“Tuzo hii ni ishara ya mafanikio kwa taasisi yetu kwamba juhudi tunazozifanya zimekuwa na msaada mkubwa kwa jamii hususani ile ya vijijini…wito wangu kwa vijana wote wa kike na wa kiume ni kwamba watumie tuzo tuliyoipata kama fundisho la wao kutowaza kukimbilia mijini kutrafuta maisha bora na badala yake wakae na kuangalia katika maeneo yao kuna fursa gani zitakazowasaidia kuinua kipato chao,” amesema mwanamama huyo jasiri.

Bi. Rimoy amewataka vijana kufikiria mara mbili mbili hasa wanapokuwa na nia ya kuja mijini wanakuja wakiwa na malengo gani na kwamba wamebeba kitu gani kama bidhaa ambacho wakifika mijini kitawafanya wainuke kimaisha.

“Kuja mijini sio dhambi na kila mtu ana haki ya kufanya hivyo, lakini cha msingi ni kwa wao kujiuliza kuwa mbali ya nguo wanazobeba kwa ajili ya kuvaa ni bidhaa gani nyingine wanachukua ambayo wakifika mjini itakuwa ndio mtaji kwa maisha yao badala ya kuja na kuwa tegemezi na wakati mwingine kujikuta wakiangukia katika makundi hatarishi,” ametahadharisha mwanamama huyo.