Jumatano , 18th Mei , 2016

Wafanyabiashara wanawake nchini wamekuwa hawanufaiki ipasaavyo na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika masoko ya nchi jirani, licha ya Tanzania kupakana na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake nchini Tanzania Bi. Jacqueline Maleko

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake nchini Tanzania Bi. Jacqueline Maleko, amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali juu ya mbinu za kuchangamkia masoko ya bidhaa nje ya nchi, mafunzo yaliyoandaliwa na Chemba ya Wanawake Wajasiriamali au kwa kifupi TWCC kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa – UN Women.

Mjasirimali kutoka mkoani Dodoma ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Shanael Lema, amesema umri sio kikwazo cha kushiriki shughuli za uzalishaji mali na kuwataka wanawake hususani wenye umri mkubwa kuendelea kutafuta ili kuweka akiba ya kipato kwa ajili ya kizazi cha baadaye.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wanawake Wajasiriamali, Bi. Flora Rimoy amezungumzia umuhimu wa kuwaendeleza wanawake kiuchumi na faida zake kwa mustakbali wa uchumi ambapo amesema wanawake nchini wamekuwa chachu ya uanzishwaji wa biashara pamoja na viwanda vidogo vidogo.