THRDC yalaani kukamatwa wanachama wake

Sunday , 16th Jul , 2017

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC) umeeleza kusikitishwa na tukio la kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa Bi. Anna Mushi na Nicodemus Ngelela, kutoka asasi ya kiraia ijulikanayo kama Action for Democracy and Local Governance ADLG

Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa.

Watu hao wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka wakiwa katika majukumu yao ya kawaida huko wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hii leo, Mratibu wa Kitaifa wa mtandao huo Bw. Onesmo Olengurumwa, amesema wanachama hao wa (THRDC) wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka wakati wakitekeleza majukumu yao ambapo ameiomba Jamhuri kufuta kesi inayowakabili wanaharakati hao.

Aidha, Bw. Olengurumwa ameziomba mamlaka za wilaya na mikoa kubadili mtazamo walionao kuhusu majukumu ya asasi za kiraia, kutokana na kile ilichokiita kuwa ni ongezeko la matukio ya kuminywa kwa uhuru wa kukusanyika na kujieleza ambapo katika baadhi ya maeneo watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakikamatwa na kuwekwa kizuizini.