Jumatatu , 5th Jan , 2015

Mbunge wa Kigoma kusini, David Kafulila, wale wanaojaribu kumkingia kifua Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo pamoja na watuhumiwa wengine ili wasiwajibishwe wanajisumbua.

Mhe. David Kafulila

Kafulila amesema Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alipewa muda wa zaidi ya saa moja kujitetea bungeni lakini akashindwa kuwashawishi wabunge kuwa hakuhusika na wizi wa fedha hizo, hivyo wale wanaojaribu kumkingia kifua ili Rais Jakaya Kikwete asimuwajibishe wanajisumbua.

Akihutubia mkutano wa hadhara ambao umeandaliwa na vyama vya vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, na kuhuduriwa na mamia ya wananchi katika maeneo ya Uyole jijini Mbeya, Kafulila amesema kuwa maazimio ya Bunge ya kutaka watuhumiwa wa sakata la Escrow wawajibishwe yapo palepale.

Amesema wale wanaojaribu kumtetea waziri wa nishati na madini Prof. Sospeter Muhongo wanahangaika bure kwa vile Prof. Muhongo mwenyewe alishindwa kujitetea bungeni licha ya kupewa muda wa kutosha wa kujitetea.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya, Joseph Mwachembe maarufu kwa jina la China amesema kuwa amebaini kuwa wakurugenzi wote wa halmashauri mkoa wa Mbeya wamepewa maelekezo ya siri ya kuandaa mahali pa kujiandikishia kupiga kura, hivyo amewataka wananchi kuwa makini na kujitokeza kwa wingi punde zoezi la kujiandikisha litakapoanza.

Mbunge mstaafu wa jimbo la Mbeya mjini kupitia chama cha NCCR mageuzi, Policia Mwaiseje amesema kuwa wananchi hawana sababu ya kusoma Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa imeandikwa na mafisadi wa Escrow na badala yake wakaikatae kwa kuipigia kura ya hapana.