Jumatatu , 6th Mei , 2024

Jeshi la Polisi wilayani kilosa limewatia mbaroni watu wawili akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msowero A, Petro Sanga (Paroko) mwenzake, Awadh Ngajime kwa tuhuma za kuuza ardhi  (eneo la mlima) mali ya kijiji cha Msowero, wilayani Kilosa.

Baadhi ya Wanachi wa Kata ya Msowero, wakiwa Katika Mkutano wa Hadhara na Mkuu wa Wilaya

Pia, inaendelea kuwatafuta watu wengine 48 ambao wanaosadikiwa kuwa sehemu ya mtandao uliohusika kuuza kinyume na utaratibu ekari 1158 za Kijiji zilizopo katika mlima huo.

Hayo yalibainika wakati wa mkutano wa hadhara kusikiliza kero za wanachi katika Kata ya Msowero uliotishwa na Mkuu wa Wilaya ya KIlosa Shaka Hamdu Shaka mwishoni mwa wiki kijjijini hapo.

Shaka alisema kumekuwa na wimbi la uvamizi wa maeneo ya ardhi unaoonekana kukithiri siku hadi siku na baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakihusika kuyauza kinyume na sheria.

"Tuna kata saba ndani ya wilaya hii zinaongoza kwa migogoro ya ardhi ikiwemo hii ya Msowero mnaongoza mnavamia maeneo ya serikali, viongozi wapo mnashirikiana nao wengine kisha mnageuka mnasingizia viongozi wa wilaya mkoa na taifa kuwa wanakuja kupora ardhi yenu kumbe ni uongo kabisa.

"Mmeuza mlima kinyume na utaratibu ekari 1,158 zote mmevamia na kuuza hii ni mali ya serikali ya kijiji kisha mnageuka kushutumu wengine kumbe wenyewe ndio wahusika, Ocd Huyu mwenyekiti wa kitongoji aliyeshiriki kuratibu mauziano na na kukiri mbele yangu kuwa  amelipwa T.  shs 500,000 na huyu aliuza eneo la mlima kwa sh 20,000,000 naondoka nao, pia naagiza watu wengine 48 waliohusika kwenye kuuza wajisalimishe vinginevyo watafutwe popote walipo na wafikishwa kwenye vyombo vya sheria," alisema

Hata hivyo, Shaka alipiga marufuku na kuweka zuwio la kuendeleza shuhuli yoyote katika eneo la mlima unaodaiwa kuuzwa huku akisisitiza kuwa walioziwa maeneo hayo wametapeliwa na mlima huo bado ni mali ya Serikali.

"Viongozi mpo mnayaona kitongoji, kijiji, kata wote mnajua lakini mnalea uovu huu, haiwezekani kila aliyehusika kwenye hili hatabaki salama ili iwe fundisho kwa wengine, naomba wajuilisheni wote walionunua eneo lile wametapeliwa na hatutasita kuchukua hatua kwa yoyote atakaekaidi amri halali ya serikali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msowero Abdalla Machera alimueleza mkuu wa wilaya kuwa katika siku za karibuni viongozi wa kisiasa wamekuwa wakifika katika maeneo yao huku wakilazimisha wananchi kupigwa picha na kutoa malalamiko ama shutuma za uongo  dhidi ya serikali jambo ambalo amesema sio la kiungwa na kistarabu.

"Mhe DC unayoyasikia huko ni kutaka kuchafua kata yetu na viongozi wetu ninyi ili wao kutafuta kuungwa mkono kwa mambo ya uongo na uzushi, yaliopo hapa ni baadhi ya wananchi kujihusisha katika matendo maovu sasa wakiona mnataka kuwachukulia hatua wanakimbilia kwa viongozi wa kisiasa ili wapaze sauti wakidhania wanaweza kuzima uovu wao wasichukuliwe hatua kwa makosa  yao, haiwezekani, wameuza mlima wetu ekari 1158 tinaomba tusaidie" Alisema   Mwenyekiti  wa kijiji Msowero

Jumla ya wananchi 50 wanadaiwa kuhusika katika kuuza Mlima Gongwe wenye ukubwa wa ekari 1158 kwa watu mbali mbali kutoka nje ya wilaya kwa shuhuli za kilimo na ujenzi wa makaazi na wengine kuvamia kuweka maakazi na kilimo ambapo imebainika pia kufanyika kwa uharibifu mkubwa wa mazingira.