Jumatano , 18th Nov , 2020

Kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP), na mgombea urais wa Uganda, Robert Kyagulanyi, maarufu kwa jina la Bobi Wine,amekamatwa mapema leo Novemba 18, 2020, na jeshi la polisi nchini Uganda, akiwa katika harakati zake za kufanya kampeni.

Mgombea urais wa Uganda Bobi Wine

Mbunge huyo wa Kyadondo Mashariki, amekamatwa Jumatano ya leo kufuatia mzozo kati ya wafuasi wake na watendaji wa usalama katika eneo lake la kampeni.

Imedaiwa kuwa kukamatwa kwa Bobi Wine, kumekuja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo IGP Martin Okoth Ochola, kumuonya kwamba amekuwa akikaidi miongozo ya uchaguzi yenye nia ya kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa wa COVID-19.

"Licha ya maonyo yanayotolewa mara kwa mara kwa wagombea, mawakala wao na umma kwa ujumla juu ya athari mbaya na hatari za kiafya za kufanya mikutano na maandamano yasiyoruhusiwa, tunaendelea kushuhudia vitendo vya kukaidi na kupuuza kabisa miongozo ya EC, kwahivyo wale watakaokaidi miongozo hii ya Tume ya Uchaguzi na mipango yao mibaya inayolenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi watawajibishwa", amesema IGP Ochola.

Aidha imedaiwa kuwa Bobi Wine, katika siku za nyuma ameonekana akihutubia umati wa watu bila kuchukua tahadhari na miongozi ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19, akiwa katika harakati zake za kutaka kumuondoa Rais wa Yoweri Museveni ambaye ameliongoza Taifa hilo tangu mwaka 1986.

Chanzo: Daily Monitor