Jumapili , 22nd Oct , 2017

Klabu ya soka ya Yanga imejibu salamu za Simba za jana baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Stand United kwenye mchezo uliomalizika jioni hii uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Nyota wa mchezo huo alikuwa ni Ibrahim Ajib ambaye aliandikia Yanga bao la mapema kupitia mkwaju wa adhabu ndogo dakika ya 24 ambao ulienda moja kwa moja golini. Baadae dakika ya 30 Ajib aliongeza bao la pili na kufanya timu hizo ziende mapumziko Yanga ikiongoza kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili Yanga walirejea na kasi ileile wakiendelea kushambulia lango la Stand United ambapo dakika ya 53 kiungo mpya wa timu hiyo Pius Buswita aliipatia bao la tatu timu yake kabla ya Obrey Chirwa kukamilisha majibu ya Yanga kwa Simba kwa kufunga bao la 4 dakika ya 69.

Baada ya mchezo nahodha wa mabingwa watetezi wa timu hiyo Nadir Haroub amesema matokeo hayo yamewaweka tayari kwaajili ya mchezo wa watani wa jadi jumapili ijayo kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

“Tunajisikia vizuri kwa matokeo haya ni maandalizi mazuri ya mchezo wetu na Simba na kila mchezaji atakaye pata nafasi ataiwakilisha Yanga vizuri”, amesema Nadir.

Yanga sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya Simba zote zikiwa na alama 15 zikitofautiana mabao ya kufunga huku Mtibwa Sugar nayo ikiwa kwenye nafasi ya 3 ikiwa na alama 15 sawa na Simba na Yanga ikizidiwa mabao ya kufunga. Mchezo wa wikiendi ijayo ndio utaamua nani aongoze msimamo wa ligi.