Saturday , 6th Jun , 2015

Dkt Mohamed Gharib Bilal amewaongoza mamia ya wakazi wa jimbo la Ukonga katika maziko ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam, Mh. Eugen Mwaiposa yaliyofanyika nyumbani kwake Kipunguni B jijini Dar es Salaam.

Jeneza lenye mwili wa marehemu muda mfupi kabla ya maziko

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Mohamed Gharib Bilal amewaongoza mamia ya wakazi wa jimbo la Ukonga katika maziko ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam, Mh. Eugen Mwaiposa yaliyofanyika nyumbani kwake Kipunguni B jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali wa chama na serikali wamehudhuria maziko hayo ikiwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda kwa niaba ya wabunge wote.

Viongozi wengine ni naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angela Kairuki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki, Waziri wa TAMISEMI Mh Hawa Ghasia, Waziri wa Maendeleo ya jamii jinsia na watoto Mhe. Sophia Simba, pamoja na wabunge mbalimbali wakiwemo Emmanuel Nchimbi na Shamsi Vuai Nahodha,

Wakimzungumzia marehemu, Mh. Simba amesema kuwa yeye pamoja na wabunge wengine wameshtushwa sana na kifo hicho cha ghafla na wanatoa pole kwa wananchi wa jimbo la ukonga kwa kuwa wameondokewa na mtu muhimu ambaye alikuwa mbunifu, mchapakazi na alikuwa karibu nao katika kuwainua kiuchumi hususani kupitia SACCOS na kuwawezesha vijana wa bodaboda.

Mh Simba amesema “Kwa siku tatu tulizokaa hapa tumeshuhudia ni kwa jinsi gani Mwaiposa alikuwa anapendwa na wananchi wake, na hata sisi wabunge wa Dar es salaam tumeondokewa na mshauri muhimu sana…”

Kwa upande wake Mh. Ghasia amesema kuwa ameondokewa na mjumbe makini wa kamati ya TAMISEMI “alikuwa anajenga hoja, alikuwa si mtu wa kuongea hovyo, pia tulikuwa tukikutana katika mazoezi na alikuwa ana bidii sana, alikuwa hakosi mazoezini baada ya Gym ya bunge kuanzishwa”

Ghasia ameongeza kuwa “Marehemu alikuwa ni mtu wa mwisho mimi kuzungumza naye, aliniuliza kwanini siendi mazoezi nikamwambia nimeshauriwa na daktari, na kuna mambo tulikubaliana pamoja na Betty Machangu kwamba nikirudi kutoka Mtwara tuyatimize lakini imekuwa tofauti…”

Tags: