Friday , 15th May , 2015

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya kuogelea Alex Mwaipasi amesema ameridhishwa na viwango vya waogeleaji wa timu ya taifa iliyoshiriki michuano ya kanda ya nne iliyofanyika jijini Luanda, Angola.

Akizungumza na East Africa Radio, Mwaipasi amesema waogeleaji hao walifikisha muda binafsi ambao ulikuwa mzuri katika mashindano hayo ambapo wamepata medali moja ya dhahabu na ya shaba.

Mwaipasi aliwataja waogeleaji waliopata medali kuwa ni Josephina Oosterhuis aliyepata medali ya dhahabu na Smriti Gorakn aliyepata medali ya shaba.

Mwaipasi amesema, licha ya waogeleaji hao kufikisha muda mzuri lakini timu hiyo iliweza kushika nafasi ya nane kwa upande wa wanawake na nafasi ya tisa kwa upande wa wanaume kutokana na kuwa na idadi ndogo ya waogeleaji ukilinganisha na nchi nyingine shiriki zilizowakilishwa na waogeleaji wengi zaidi.