Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, katika mkutano wake na wadau wa uhifadhi na wanyamapori kutoka sehemu mbalimbali nchini, mkutano uliohusisha pia nchi wahisani, asasi za kiraia pamoja na mashirika yanayojihusisha na uhifadhi.
Waziri Nyalandu amesema athari ya ujangili inaonekana zaidi katika hifadhi ya Selous ambako takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa idadi ya tembo imepungua kutoka elfu thelathini na tisa hadi kufikia tembo elfu kumi na moja.
Waziri Nyalandu amesema ni jukumu la wananchi wote kuhakikisha kuwa wanashiriki katika mapambano dhidi ya ujangili na ambapo kwa upande wake ametaja hatua kadhaa zinazochukuliwa kudhibiti ujangili.
Moja ya hatua hizo kwa mujibu wa waziri Nyalandu ni pamoja na majaribio juu ya matumizi ya ndege maalumu zisizo na rubani maarufu kama Drone, zitakazotumika kwa ajili ya doria katika mbuga na misitu mbalimbali ya hifadhi hapa nchini.
Aidha, amesema katika kukabiliana na uvunaji holela wa misitu, wizara yake imepanga kusaini makubaliano maalumu na serikali ya Zambia, ambapo Tanzania haitaruhusu uingiaji wa mbao kutoka nchini humo.
Makubaliano kama hayo yatasainiwa pia na nchi ya Msumbiji ambapo nchi hizo zitakubaliana kufungua ushoroba unaotumiwa na wanyamapori wanaohamahama kutoka nchi moja kwenda nyingine ili kuruhusu wanyamapori wanaoishi na kusafiri kati ya mbuga ya Nyasa pamoja na hifadhi ya Selous.
Katika makubaliano na nchi ya Zambia, waziri Nyalandu amesema uchunguzi wao umebaini kuwa baadhi ya majangili wamekuwa wakiingia katika misitu ya Tanzani katika mipaka jirani na nchi hizo ambako wamekuwa wakivuna na baadaye kuingia nayo nchini wakijifanya kwamba imetokea nchini Zambia.