Sunday , 15th Mar , 2026

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetolea ufafanuzi tukio la mauaji ya watu wanne na majeruhi mmoja lililotokea katika kilabu cha pombe za kienyeji huko Kiwangwa wilayani Bagamoyo Machi 12, 2026 majira ya saa 20.45 usiku huko maeneo ya Kidudumale Mwetemo baada ya mtu mmoja aliyefahamika kwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetolea ufafanuzi tukio la mauaji ya watu wanne na majeruhi mmoja lililotokea katika kilabu cha pombe za kienyeji huko Kiwangwa wilayani Bagamoyo Machi 12, 2026 majira ya saa 20.45 usiku huko maeneo ya Kidudumale Mwetemo baada ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Boniphace Ikilala Ndalemi maarufu kama Swai (53) Muha, mkazi wa Kidudumale kuwakata kwa panga watu watano.

Awali, Mtuhumiwa alifika kilabuni hapo majira ya saa 11:00 jioni na kuagiza pombe ya kienyeji inayofahamika kwa jina la Mabuya akanywa na kuondoka eneo hilo kuelekea kusikojulikana na ilipofika majira ya saa 2:15 usiku alirudi tena kilabuni akimdai mmiliki wa kilabu hicho Bi. Asha Khamis Athuman kiasi cha shilingi 5000 ambayo alieleza kuwa aliiacha alipofika kilabuni hapo kwa mara ya kwanza.

Mtuhumiwa alianza kuzozana na mmiliki wa kilabu hicho cha pombe kuhusu pesa hiyo na baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walikua wakimsaidia Asha Khamis kuwa Boniphace Ndalemi hakuacha pesa ya ziada alipofika kilabuni hapo kwa mara ya kwanza. Boniphace Ndalemi alianza kuwashambulia watu hao kwa panga maeneo ya kichwani.

Mara baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kupata taarifa hiyo lilifika eneo la tukio na katika jitihada za kumkamata mtuhumiwa huyo alikaidi amri za Polisi na kuendelea kuhatarisha usalama wa askari na wananchi waliokuwepo eneo hilo hali iliyosababisha askari kumpiga risasi mguu wa kulia hivyo akaanguka chini. Mtuhumiwa huyo alifariki akiwa njiani akipelekwa kituo cha Afya Kiwangwa.