Wananchi wa Kijiji cha Lowe kilichopo Kata ya Lusaka, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wanakabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa daraja la uhakika, hali inayohatarisha usalama wao na kuathiri shughuli za kila siku.
Kwa mujibu wa wananchi hao, Kivuko kinachotumika kwa sasa kimejengwa kwa nguvu za wananchi bila kuzingatia viwango sahihi, hali inayowaweka hatarini watumiaji wake hususan kipindi cha mvua.
Aidha, wamesema tayari wametumia zaidi ya shilingi milioni 9 zilizotokana na michango yao binafsi kwa ajili ya ujenzi wa kivuko hicho, hata hivyo bado hakijakidhi mahitaji kwa matumizi.
Diwani wa Kata ya Lusaka, Julius Boymanda, ametembelea eneo hilo na kushuhudia jitihada za wananchi katika kujiletea maendeleo, akibainisha umuhimu wa serikali kuingilia kati ili kusaidia upatikanaji wa daraja la kudumu.
