Mkuu wa mkoa wa Kagera, Hajati Fatuma Mwassa amewaongoza wakazi wa mkoa huo katika sala na Dua ya kuombea taifa na mkoa wa Kagera, ikiwa ni mwanzo wa tamasha la ijuka omuka, ambalo linafanyika kuanzia Leo na kuhitimishwa Desemba 21 mwaka huu katika uwanja wa Kaitaba.
Sala na Dua hiyo imeongozwa na mkurugenzi wa idara ya utume wa walei Jimbo katoliki la Bukoba, padri Philbert Mutalemwa, mchungaji Godlove Mweyunge na shekhe wa mkoa wa Kagera,Haruna Kichwabuta.
Tamasha hilo ambalo hufanyika Desemba kila mwaka, lilibuniwa na serikali ya mkoa, likilenga kuwakutanisha wazawa wanaoishi ndani na nje, ili kuwaelezea fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo, na kuwatambua wanakagara ulioshiriki katika kuchochea maendeleo ya mkoa.
Tamasha la Ijuka Omuka, ambao tafsiri yake ni kumbuka nyumbani, kwa mwaka huu limeonekana kuja kitofauti,baada ya kuongezewa vionjo vinavyotajwa kama kivutio, ikiwemo mchezo kati ya viongozi wa serikali ambao ni wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wa dini.
