Sunday , 7th Dec , 2025

Msemaji wa polisi Brigedia Athlenda Mathe amesema watu watatu wenye silaha wasiojulikana waliingia katika baa hiyo ambapo kundi la watu walikuwa wakinywa vinywaji na kufyatua risasi ovyo.

Watu 11 wameuawa kwa kupigwa risasi huku wengine kumi na wanne wakijeruhiwa katika baa moja nchini Afrika Kusini baada ya watu wenye silaha kuvamia jengo hilo, katika mji wa Saulsville, magharibi mwa mji mkuu Pretoria, mapema jana Jumamosi asubuhi.

Msemaji wa polisi Brigedia Athlenda Mathe amesema watu watatu wenye silaha wasiojulikana waliingia katika baa hiyo ambapo kundi la watu walikuwa wakinywa vinywaji na kufyatua risasi ovyo.

Watu hao wenye silaha wanaripotiwa kuingia katika jengo hilo saa 10:30 alfajiri kwa saa za huko na kufyatua risasi kwa kundi la wanaume waliokuwa wakinywa pombe. Mvulana wa miaka 12 na msichana wa miaka 16 ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo.

Bado sababu za kitendo hicho hazijulikani, na hakuna mtu aliyekamatwa katika tukio la hivi karibuni zaidi kwenye mfululizo wa matukio ya ufyatuaji risasi wa watu wengi nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

"Ninaweza kuthibitisha kwamba jumla ya watu 25 wamejeruhiwa kwa risasi," Mathe amesema huku mtoto wa miaka mitatu akitajwa pia kuwa ni miongoni mwa waathiriwa.

Baa hiyo ambayo imetajwa kama sehemu ya unywaji pombe haramu, imetajwa kuwa ni miongoni tu mwa sehemu zinazouza pombe kinyume cha sheria na bila leseni, ambapo, mauaji mengi ya watu wengi hutokea.

Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, ikiwa na vifo 45 kwa kila wakazi 100,000, kulingana na takwimu za mwaka 2023-2024 kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu.