Monday , 27th Oct , 2025

Wanamgambo kutoka kundi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin linaloungwa mkono na al-Qaida walitangaza kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka nchi jirani kuingia Mali mapema Septemba, wakikandamiza uchumi dhaifu wa nchi hiyo isiyo na bandari.

Nchi ya Mali imefunga shule na vyuo vikuu kote nchini humo kuanzia jana Jumapili kutokana na uhaba wa mafuta uliosababishwa na kizuizi cha uagizaji wa mafuta kilichowekwa na wanamgambo wa jihadi katika mji mkuu.

Waziri wa Elimu Amadou Sy Savane almeangaza kwenye televisheni ya serikali kwamba madarasa yangesimamishwa kwa wiki mbili kutokana na usumbufu wa usambazaji wa mafuta unaoathiri harakati za wafanyakazi wa shule. Amesisitiza kuwa mamlaka zinafanya kila linalowezekana kurejesha usambazaji wa kawaida wa mafuta kabla ya shule kuanza tena madarasa Novemba 10.

Wanamgambo kutoka kundi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin linaloungwa mkono na al-Qaida walitangaza kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka nchi jirani kuingia Mali mapema Septemba, wakikandamiza uchumi dhaifu wa nchi hiyo isiyo na bandari na kuacha mamia ya malori ya mafuta yakiwa yamekwama mpakani.

Mali, pamoja na nchi jirani za Burkina Faso na Niger, inapambana na uasi wa makundi yenye silaha, ikiwa ni pamoja na baadhi ya washirika wa al-Qaida na kundi la Islamic State pamoja na waasi wa eneo hilo. Kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika mataifa yote matatu katika miaka ya hivi karibuni, wamewafukuza wanajeshi wa Ufaransa na kugeukia vitengo vya mamluki vya Urusi kwa usaidizi wa usalama, ambao wachambuzi wanasema haujaleta tofauti kubwa.

Katika mji mkuu wa Mali, Bamako, foleni zisizo na mwisho zimeenea mbele ya vituo vya mafuta na uhaba wa mafuta umeathiri bei ya bidhaa na usafiri. Kwa nchi inayotegemea uagizaji wa mafuta kwa mahitaji ya ndani kama Mali, kizuizi hicho kinaonekana kama kikwazo kikubwa kwa utawala wa kijeshi wa Mali.

Kufuatia uhaba huo Jeshi la Mali lilijaribu kusindikiza baadhi ya malori ya mafuta kutoka maeneo ya mpakani hadi Bamako. Baadhi ya malori yalifika lakini mengine yalishambuliwa na wanamgambo.

Itakumbukwa kuwa utawala wa kijeshi nchini Mali umetetea utwaaji wake wa nguvu wa madaraka mwaka wa 2020 kama hatua muhimu ya kukomesha miongo kadhaa ya migogoro ya usalama.