Friday , 24th Oct , 2025

“Tunakwenda Mahakama Kuu kuomba itamke kwamba kitendo cha wananchi wa Kigamboni au mtu yeyote kutoka nje ya Kigamboni kulazimika kulipa tozo ya kuvuka daraja hilo ni kinyume cha Katiba.”

Wakili Mohamed Majaliwa kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania amesema anapanga kufungua kesi ya Kikatiba kwa niaba ya wananchi wa Kigamboni akiiomba Mahakama itoe tamko kuwa tozo ya kuvuka Daraja la Kigamboni ni kinyume cha Katiba.

Akizungumza leo Oktoba 24 jijini Dar es Salaam, Wakili Majaliwa amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kutumia njia mbalimbali kutatua changamoto hiyo bila mafanikio ili kuondoa kile alichokiita mzigo wa kikatili kwa wananchi wa Kigamboni.

Majaliwa ameongeza kuwa utaratibu wa sasa wa kutoza tozo hizo unakinzana na sheria zenyewe zinazotumika, ambazo ni Kanuni ya Tozo za Barabara ya mwaka 1985 (The Road Tolls Fees Regulations, 1985) na Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta (The Road and Fuel Tolls Act) akisema hazielekezi wananchi kulipa kodi mara mbili kwa matumizi ya miundombinu ya barabara, lakini mfumo wa sasa wa tozo za daraja hilo unasababisha wananchi wa Kigamboni kulipa kodi mara mbili kupitia kodi ya mafuta na tena kupitia tozo ya kuvuka daraja.

“Ukizisoma sheria hizi mbili kwa pamoja, mimi kama mkazi wa Kigamboni nikitumia daladala au gari binafsi, nalazimika kulipa kodi mara mbili. Hili ni kinyume na misingi ya usawa na haki kwa mujibu wa Katiba,” amesema Majaliwa.

“Tunakwenda Mahakama Kuu kuomba itamke kwamba kitendo cha wananchi wa Kigamboni au mtu yeyote kutoka nje ya Kigamboni kulazimika kulipa tozo ya kuvuka daraja hilo ni kinyume cha Katiba,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya serikali kuzindua Dira ya Maendeleo ya Miaka 25, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kupunguza au kuondoa tozo hiyo kwa wananchi wa Kigamboni, jambo alilosema linazidi kuwa kero kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na wageni wanaotumia daraja hilo kila siku.