Sunday , 5th Oct , 2025

Mawaziri hao wamekubaliana kuanzisha mfumo wa mashauriano ya kisiasa na kiuchumi ili kuweka msingi imara wa ushirikiano wa kimkakati kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa mataifa hayo mawili. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufalme wa Sweden, Mhe. Maria Malmer Stenergard, pembezoni mwa Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe tarehe 2 na 3 Oktoba 2025.

Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Sweden katika siasa, uchumi, nishati na maendeleo ya watu. Waziri Kombo ameishukuru Sweden kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania, hasa katika sekta za elimu, afya, nishati, utawala bora na maendeleo ya jamii.

Amesema Tanzania inatambua uhusiano huo wa kihistoria na ina dhamira ya kuuendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili. Aidha, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara na uwekezaji badala ya kutegemea misaada, huku akiikaribisha Sweden kuwekeza zaidi katika sekta za nishati jadidifu, TEHAMA, kilimo, viwanda na utalii.

Ameeleza kuwa Tanzania inalenga kufikia upatikanaji wa nishati kitaifa kwa asilimia 85 mwaka 2025 na hivyo inakaribisha ushirikiano katika miradi ya nishati safi na endelevu.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Mhe. Stenergard, ameipongeza Tanzania kwa kudumisha amani, utawala bora na sera zake za kukuza uchumi jumuishi. Amesema Sweden inatambua nafasi ya Tanzania kama nguzo muhimu ya amani na maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Waziri Stenergard ameahidi kuwa Sweden itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza demokrasia, maendeleo ya kijamii na miradi ya nishati mbadala. Amesema makampuni ya Kiswidi yana nia ya kuwekeza zaidi nchini Tanzania, hasa katika miundombinu, madini, usafiri na huduma za afya.

Mawaziri hao wamekubaliana kuanzisha mfumo wa mashauriano ya kisiasa na kiuchumi ili kuweka msingi imara wa ushirikiano wa kimkakati kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa mataifa hayo mawili.