
Naibu Waziri wa Madini Stephen Kiruswa amesema watu 21 bado hawajaokolewa kwenye mashimo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Nyandolwa kijiji cha Mwongozo ambayo yametitia, huku mmoja kati ya wanne waliookolewa, Emanuel Kija (27) akifariki dunia.
Naibu Kiruswa ameyasema hayo jana Agosti 12,2025 alipotembelea eneo hilo ambapo watu 25 walifukiwa huku jitihada za uokozi zikiendelea ambapo watu wanne wamekolewa mpaka sasa akiwemo mmoja aliyefariki huku wengine watatu hali zao zikiendelea vizuri baada ya kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Kiruswa amesema zoezi la uokoaji linaendelea kufanyika kwa umakini ili kuwatoa watu 21 ambao bado wapo chini, kwa imani kuwa bado wako hai. "Tunaendelea na juhudi za uokoaji usiku na mchana , hata kama tutawapata wakiwa wamekufa au hai lazima wote tuwatoe, na tayari nimetoa maelekezo vifaa vyote muhimu vya kutolewa huduma ya kwanza,mitungi ya hewa ya Oxygen iwepo" amesema Kiruswa.
Aidha Kiruswa amesema maduara ya eneo hilo yamekaribiana kuta zake ndiyo maana mashimo hayo yalikuwa yakifanyiwa ukarabati. Pia amezitaka amlaka zinazosimamia kwa kushirikiana na Tume ya Madini ziwaelekeze na kuwashauri wachimbaji ili kupunguza maafa yanayotokea migodini.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro amewataja waliookolewa kuwa ni Furano Peter, Antony Clement ,Nugula Japhet na Emanuel Kija ambaye alifariki baada ya hali yake kuwa mbaya, pamoja na kuwekewa mtungi wa Oxgen.
Mtatiro amesema kuna shimo la duara 106 ambalo kulikuwa na watu sita lina mita 130 kwenda chini na walitoa miili ya watu wanne na shimo duara 20 lilikuwa na watu wanane lina mita 85 kwenda chini na hawajatoa mtu hata mmoja lakini waokoaji wamelikaribia bado mita 15 kuwafikia mpaka sasa, pia, amewataka ndugu na jamaa kuwa wavumilivu na kutokuwa na hofu zoezi la uokoaji likiendelea.