Thursday , 10th Jul , 2025

Kundi la Hamas limesema litawaachilia mateka 10 wanaowashikilia kama msingi wa sehemu ya mazungumzo ya kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, baada ya Israel kusisitiza matarajio ya kufikia makubaliano

Hamas imetoa kauli hiyo baada ya siku nne za mazungumzo yanayofanyika kupitia kwa wasuluhishi, yanayosimamiwa na Qatar.

Marekani pia imeashiria imani kwamba makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa muda wa siku 60 yanaweza kufikiwa kabla ya mwisho wa wiki hii. 

Hata hivyo Hamas imesema bado kuna vizingiti vikubwa kwenye mazungumzo na hasa suala la upatikanaji wa misaada kwenye Ukanda wa  Gaza, kuondoka kwa jeshi la Israel kwenye eneo hilo na kuhakikishiwa kuwepo amani ya kudumu.

Mjumbe maalum wa Marekani, wa maswala ya Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, amesema sehemu ya mpango huo itakuwa ni kuachiwa kwa mateka hao 10 ambao bado wapo hai wanaoshikiliwa na Hamas tangu mwezi Oktoba, mwaka 2023.

Wakati huo huo shirika la ulinzi wa raia kwenye Ukanda wa Gaza limesema watu 23 wakiwemo watoto wanane, wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na Israel usiku wa kuamkia leo.