Tuesday , 17th Jun , 2025

Mashambulizi ya anga kati ya Israel na Iran yameingia siku ya tano, huku idadi ya vifo ikiongezeka, watu wanakimbia makazi yao, na diplomasia ikivurugika hali inayochochea hofu ya kuzuka kwa vita vya kikanda kwa kasi.

Israel na Iran zimeendelea kurushiana makombora kwa siku ya tano mfululizo katika kile kinachoelezwa kuwa makabiliano ya moja kwa moja na yenye ukali zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya mahasimu hao wawili.

Kutoka kwa vita vya uwakala na operesheni za siri, hali sasa imebadilika na kuwa vita vya wazi – hali inayozua hofu kubwa ya kuibuka kwa vita vikubwa katika Mashariki ya Kati.

Israel ilitangaza Jumanne kwamba ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya vituo vya droni na makombora magharibi mwa Iran, hasa katika jiji la Tabriz.

Milipuko pia ilisikika mjini Tehran na Natanz, maeneo yenye mitambo ya nyuklia. Iran ilijibu kwa mashambulizi mapya ya droni na makombora, huku kamanda wake Kiumars Heydari akisema yataongezwa ukubwa.

Wakati huo huo, Iran imeripoti vifo vya watu wasiopungua 224 na zaidi ya 1,200 kujeruhiwa, huku Israel ikithibitisha vifo vya raia 24 na kuwahamisha zaidi ya watu 3,000.

Miji ya Tel Aviv na Jerusalem imeshuhudia tahadhari za mashambulizi huku vipande vya makombora vikisababisha uharibifu.

Jeshi la Israel linasema limeharibu theluthi moja ya mifumo ya makombora ya Iran na kumuua mkuu wa majeshi wa wakati wa vita. Msemaji wa jeshi Effie Defrin alidai kuwa sasa Israel inadhibiti anga ya Tehran.

 Hata hivyo, vyombo vya habari vya kimataifa vimeripotiwa kukabiliwa na vikwazo nchini Israel katika kuripoti mashambulizi hayo.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema kampeni ya kijeshi inalenga kusambaratisha mpango wa nyuklia wa Iran, uwezo wake wa kutengeneza makombora, na kuangamiza mitandao ya ugaidi. Alidokeza pia uwezekano wa kulenga viongozi wa ngazi ya juu wa Iran.